Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa
Ligi Tanzania au Kamati ya Saa 72, ilifanya kikao chake juzi Ijumaa
Aprili 7, 2017 jijini Dar es Salaam na kufikia uamuzi ufuatao.
Kuhusu Mchezaji Abdi Banda
Mechi namba 194 (Kagera Sugar 2 vs Simba 1). Beki
wa Simba, Abdi Banda jezi namba 24 amesimamishwa kucheza Ligi Kuu
wakati akisubiri suala lake la kumpiga ngumi kiungo wa Kagera Sugar,
George Kavilla jezi namba 15 wakati akiwa hana mpira kusikilizwa na
kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF).
Alifanya kitendo hicho ambacho
hakikuonwa na waamuzi katika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 2, 2017
kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Uamuzi wa Kamati umezingatia
Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu.
Pia Kamati ilibaini kuwa Banda alifanya
kitendo cha aina hiyo kwenye mechi namba 169 kati ya Simba na Yanga
iliyofanyika Februari 25, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Awali, Klabu ya Kagera Sugar
iliwasilisha malalamiko dhidi ya kitendo cha beki wa Simba, Abdi Banda
kumpiga ngumi kiungo wao George Kavilla wakati akiwa hana mpira, na
Mwamuzi wa mechi hiyo kutochukua hatua yoyote.
Kwa vile kosa hilo ni la kinidhamu,
Kamati imemsimamisha Abdi Banda kwa mujibu wa Kanuni ya 9(5) wakati
akisubiri suala lake kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu
ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Kamati ya Nidhamu
inatarajiwa kukaa wakati wowote wiki ijayo.
Kadhalika Klabu ya Simba iliwasilisha
malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana
na timu ya Kagera Sugar kumchezesha mchezaji Mohamed Fakhi Gharib
wakati akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao namba 194
iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Kamati baada ya kupitia malalamiko hayo,
imeahirisha shauri hilo hadi Alhamisi Aprili 13, 2017 kwa vile bado
inafuatilia baadhi ya vielelezo kuhusu malalamiko hayo kabla ya kufanya
uamuzi.
0 Komentar untuk "BEKI WA SIMBA ABDI BANDA AMESIMAMISHWA KUCHEZA LIGI KUU"