HII NDO KAULI YA MAALIM SEIF KWENDA KWA PROF.LIPUMBA KUFUATIA SUALA LA YEYE KUVULIWA MADARAKA



Sarakasi za kisiasa zinaendelea kutawala ndani ya chama cha CUF baada ya Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, kudai kuwa Profesa Ibrahim Lipumba anatumiwa kukihujumu chama hicho.

Maalim Seif alimtuhumu Profesa Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa CUF, anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuwa anakihujumu chama ili kishindwe kudai haki waliyoipata katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka juzi.

Aliyasema hayo jana katika kijiji cha Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja alipozungumza na wanachama wa chama hicho, ikiwa ni ziara maalumu ya uimarishaji wa chama katika mikoa yote ya Kisiwa cha Unguja.

Maalim Seif alisema pamoja na Profesa Lipumba kupata nguvu kutoka vyombo vya dola na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika kukihujumu chama hicho, lakini hawataweza kufikia malengo hayo.

Alisema taasisi hizo kwa pamoja zimekuwa zikimuunga mkono Lipumba kwa kumpa kila nguvu anayohitaji ili kuona anafanikisha malengo ya CCM ya kuitawala nchi bila ya kuwepo kwa chama kikuu pinzani, ila nguvu zao hizo zitagonga mwamba.

“Nashangaa sana kuona Lipumba amekubali kutumika na CCM kwa kukihujumu chama kwa masilahi binafsi, lakini nataka muelewe wananchi kuwa pamoja na nguvu zao zote hizo katu hawataweza kuwakatisha tamaa Wazanzibari ya kudai haki yao waliyoipata katika uchaguzi uliopita,” alisema.

Alishangazwa kuona Ofisi ya Msajili kwa kushirikiana na vyombo vya dola badala ya kufuata Katiba na sheria za nchi, wao wamekuwa wakikihujumu chama hicho.

“Pamoja na hujuma hizi zinazofanywa na Lipumba katika chama chetu, lakini nashangaa Rais (John) Magufuli anatumbua watendaji wabovu, lakini humu mrajisi (Msajili) wa Vyama vya Siasa anamuachia,” alisema.

Kuhusu kuondolewa kwenye nafasi yake, Maalim Seif alisema kwa mujibu wa katiba ya CUF, Lipumba hana uwezo wa kumvua nyadhifa hiyo hata kama angekuwa ni mwenyekiti halali.

Alisema kwa mujibu wa katiba yao ili Katibu avuliwe wadhifa wake lazima mkutano mkuu uhudhuriwe na zaidi ya nusu ya idadi wajumbe.

Alisema kikao kilichofanyika chini ya Profesa Lipumba kilihudhuriwa na wajumbe wasiokuwa na ujumbe kihalali, ambao walipandikizwa kuonesha kama kikao hicho kilikuwa halali.

“Ikiwa mimi nimefukuzwa chama kutokana na madai kuwa sihudhurii vikao vinavyofanywa na ofisi za chama hicho jijini Dar es Salaam, mbona yeye Lipumba tangu mwaka 2015 hawajawahi kuja ofisi kuu ya chama ambayo ni mtendeni hadi leo, kwa hiyo naye alitakiwa kufukuzwa,” alihoji.

Maalim Seif alisema kuwa kinachosikitisha ni kuona Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nayo kuidhinisha kuwa wamekubaliana na mageuzi hayo yaliyofanywa na Lipumba kwa kushirikiana na wajumbe wake.

“Ninachokifahamu mimi ndani ya katiba yetu inasema kuwa ili uamuzi wa kuvuliwa nafasi ya uongozi ni lazima anayedaiwa kufanya kosa aitwe na uongozi kujieleza, lakini mimi sijaitwa kujieleza,” alihoji Maalim Seif.

Akizungumzia madai ya kushinda Uchaguzi Mkuu uliopita, Maalim Seif alisema waliwataka wananchi wa Zanzibar kutokata tamaa na haki yao, huku akidai hivi karibuni dola ya Zanzibar itakuwa chini ya CUF.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema uongozi wa CUF unasikitika kuona vyombo vya dola vikiingilia mamlaka ya chama hicho na kusahau wajibu wao.

Alisema kuwa wajibu wa vyombo hivyo ni kusimamia amani ya wanachama na viongozi wake, lakini ni jambo la kushangaza kwa viongozi wa vyombo hivyo kuwa ni miongoni mwa wanaongoza kuonesha chuki dhidi ya CUF.

Alisema pamoja na hujuma hizo, lakini viongozi wakuu wa chama hicho chini ya Maalim Seif, hawatosita kudai haki yao hadi kieleweke.

Akijibu tuhuma hizo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho bara na anayemuunga mkono Profesa Lipumba, Magdalena Sakaya alimtuhumu Maalim Seif kuwa ndiye anakula njama za kukidhoofisha chama.

Alisema Seif amekataza ruzuku zisifike kwenye wilaya, hakuna mikutano na hakuna hata pikipiki huku wenzao Chadema waliokuja juzi wamekuwa chama kikuu cha upinzani kutokana na kuwa wamoja.

“Malalamiko anayotoa ajikite kwenye katiba, aichambue kifungu kwa kifungu atabaini anakosea wapi.

“Hii ni taasisi  ya chama, siyo kampuni ya mtu, lazima tufuate katiba tuliyojiwekea ambayo ipo wazi inatoa maelekezo ya kila kitu, anayekengeuka anafanya makusudi na sisi hatuwezi kukaa kimya bila kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuteua watakaofanya kazi alizotakiwa kufanya yeye,” alisema Sakaya.

Alieleza kuwa badala ya kujenga chama, ameamua kukidhoofisha na anatumiwa kufanya hivyo akijificha kwenye mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

“Amekuwa bwana kesi, kila kukicha anafungua mpya, mimi nina kesi, Lipumba ana kesi, Msajili wa Vyama ana kesi, mwanasheria ana kesi, akae kimya asubiri ziishe, ”alisema Naibu katibu mkuu huyo

Share :

Facebook Twitter Google+
0 Komentar untuk "HII NDO KAULI YA MAALIM SEIF KWENDA KWA PROF.LIPUMBA KUFUATIA SUALA LA YEYE KUVULIWA MADARAKA"

Back To Top