RAISI MAGUFULI:WALIOGHUSHI UMRI WAJIANDAE



RAIS John Magufuli amesema serikali imepanga kutoa nyongeza ya kila mwaka katika mishahara pamoja na promosheni baada ya kukamilika kwa uhakiki wa wafanyakazi hewa na wenye vyeti feki, huku akitangaza kuwa sasa imejipanga kufanya uhakiki wa wafanyakazi waliobadilisha umri wao wa kuzaliwa ili wasistaafu mapema.
Amesema baada ya ‘kusafisha nyumba yake’ kwa kuwaondoa watumishi hewa na walioghushi vyeti, kwa sasa mwelekeo ni mzuri na atakapopandisha mshahara atafanya hivyo kwa watumishi sahihi na ndio nia ya serikali. Amesema uamuzi wa serikali wa kuanza kutoa promosheni, unatokana na kukamilika kwa uhakiki wa wafanyakazi hewa ambao zaidi ya wafanyakazi 19,000 walibainika.
“Yale mambo yote yaliyokuwa pending ikiwa ni pamoja na promosheni kwa sababu tulishindwa, unaweza kupromoti mfanyakazi hewa, kwa sababu tungetoa promosheni wakati kuna wafanyakazi 19,000 hewa, maanake tungepromoti na 19,000 na si ajabu na watu waliowaandika mle ndio wangeletwa katika mapendekezo ya promosheni,” alisema Rais Magufuli.
Akizungumza jana kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika kitaifa kwenye Viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Rais Magufuli alisema kuna watu ambao ni wazee kwenye ofisi za umma, lakini hawataki kustaafu. Alisema mtu wa namna hiyo hana tofauti na mfanyakazi hewa kwa sababu hataki kutoka kazini ili wengine nao waajiriwe.
“Hawa ambao hawataki kuachia ofisi, lakini ni wazee, hawataki kustaafu, hao nao dawa yao inachunguzwa,” alisema Rais Magufuli na kusisitiza kuwa uhakiki wa vyeti feki na watumishi hewa umekamilika kwa asilimia 98.
Watoto wa viongozi Alisema katika watu walioghushi vyeti, kuna baadhi ni watoto wa viongozi ambao walijipatia ajira bila uhalali huku watoto wa maskini wamekuwa hawaendi kokote, licha ya kuwa na vyeti halisi. Alisema kwa sababu hiyo serikali ilisimamisha ajira kwa muda mrefu, kwa kuwa wafanyakazi walikuwa ni wengi wakiwemo hewa na wenye vyeti vya kughushi.
Rais aliwahoji wafanyakazi, “Hivi mlitaka nipandishe mishahara niwapandishie ndani humo na wale wafanyakazi hewa na watu wa kughushi vyeti, ndio maana nilitaka kwanza nisafishe nyumba. Alisema kwa sasa mwelekeo ni mzuri na atakapopandisha mshahara atafanya hivyo kwa watumishi sahihi na ndio nia ya serikali. Alisema wafanyakazi hewa, sio jipu maana halionekani, ila wafanyakazi wenye vyeti feki wapatao 10,000 ndio majipu na ameamua kuwatumbua, maana ndio walikuwepo.
Alisema ameshaagiza watu wote ambao wameorodheshwa kwenye orodha ya vyeti feki, wajiondoe ndani ya siku 15. “Waondoke hata kama ni mtoto wa waziri au wa rais, yeyote anayehusika aondoke. Akigoma apelekwe mahakamani na huko najua kifungo chao sio chini ya miaka saba,” alisema Rais Magufuli.
Hata hivyo, alisema kwamba anachojua, watumishi hao wenye vyeti feki watajiondoa tu wenyewe kwa kuwa mishahara hawataendelea kupata. Rais Magufuli alisisitiza kuwa viongozi wa juu, hawana nia mbaya kufanya uhakiki huo, bali wana nia nzuri, kwani wanataka watumishi ambao wanadai maslahi yao yaboreshwe, yaende kwa watu sahihi. Alisisitiza kuwa baada ya kuondolewa wafanyakazi hewa na wale wenye vyeti feki, serikali sasa imejipanga kuhakikisha inatoa ajira mpya kwa watu 52,000.
“Tutaajiri walimu, wauguzi na wafanyakazi wa kada zingine,” alieleza. Serikali ilivyopoteza mabilioni Rais Magufuli alisema serikali ilikuwa inapoteza Sh bilioni 19.48 kwa mwezi kwa ajili ya kuwalipa watumishi hao hewa, kama mishahara na kwa mwaka zaidi ya Sh bilioni 230 zililipwa kwa watumishi hao hewa. Rais Magufuli alisema fedha hizo, zingeweza kutumika kuwalipa wafanyakazi wanaojituma kufanya kazi usiku kucha kuliko kwenda kwa watumishi hewa.
Alishangaa kwa nini viongozi wa Tucta, hawakutoa lugha kali kwa wanachama wao, ambao walikuwa wanachangia kuwepo kwa wafanyakazi hao hewa. Alisema hatua ya kuwafuta watumishi hao hewa, imeenda vizuri na imefikia asilimia 98, lakini haijamalizika. Alisema walikuwepo watu wanaofanya kazi, lakini wana vyeti feki ambao nao serikali imeamua kuwaondoa kwenye ajira.
Alisema serikali inataka kila kazi iwe na mfanyakazi mwenye sifa stahiki na kama ni ya darasa la saba, afanye mtu mwenye elimu hiyo na sio kughushi cheti. Rais Magufuli alisema serikali imefanya uhakiki huo ili kama ni mtu wa darasa la saba, aombe kwa sifa ya cheti chake na sio kwenda kufoji cheti cha kwenda kufanya kazi ya uuguzi wakati hajafikia sifa hiyo.
Alisema kuna wakurugenzi wa mashirika na taasisi za serikali ambao wameghushi vyeti, halafu wanawanyanyasa watu wa chini ambao hawana vyeti vya kughushi. Alisema watu hao walioghushi, hawastahili nafasi hizo na ndio maana Serikali imeamua kuwaondoa. Alisema watumishi 9,932 wana vyeti vya kughushi, watumishi 1,138 wana vyeti vyenye utata kwani cheti kimoja kina watu zaidi ya mmoja.
Watumishi 11,596 waliwasilisha vyeti vya taaluma bila vyeti vya elimu. Alisema ndio maana wiki iliyopita, walichukua hatua kwa watumishi 10,000 ambao wana vyeti vya kughushi waweze kupisha ili kusudi wabaki watumishi wenye vyeti vyao. “Tunataka kama una cheti cha ualimu wewe ndio tunakuhitaji, asitokee mtu mwingine akaghushi akaenda kuwa mwalimu maana mtu huyo akienda kufundisha anaweza kupotosha na kama ni daktari anaweza kufanya operesheni kwa mgonjwa ambayo sio sahihi,” alisema Rais.
Apiga marufuku uhamisho Rais Magufuli pia alisema waliosababisha kuwepo kwa watumishi hewa wako ndani ya Serikali na walikuwa wanafaidika na hatua hiyo na kuanzia sasa amepiga marufuku mtumishi kuhamishwa bila kulipwa posho yake ya uhamisho. Alisema baadhi ya watumishi walikuwa wanawahamisha watumishi hao hewa kutoka kituo kimoja kwenda kingine ndani ya muda mfupi na fedha za uhamisho, wanajilipa wakurugenzi wenyewe.
Pia alisema kuna wakurugenzi walikuwa wanawahamisha baadhi ya watumishi wale wale kwa makubaliano ya kugawana posho za uhamisho. “Kuna mwalimu anahamishwa huyo huyo kila mwaka, kumbe huyu alikuwa na makubaliano na mkurugenzi wa kula posho ya uhamisho. “Sasa naagiza hakuna mtumishi kuhama hadi ulipwe posho ya kuhamishwa.
Hili ni agizo kuanzia ngazi ya juu hadi chini.Yeyote atakayekuhamisha wewe mtumishi, mwambie nipe hela yangu ya uhamisho kwanza ndipo niende huko unakonipeleka. Akishindwa kaa hapo hapo endelea kufanya kazi. Alisema uhamisho mwingine unafanyika kwa dhuluma na chuki. Alisema baadhi ya wakurugenzi wanawahamisha watumishi kwa kuwa na chuki ya maendeleo.
“Unakuta mwalimu umejenga kibanda chako kizuri, unahamishwa kwenda kusiko na nyumba. “Nataka wafanyakazi muishi kwa raha, awe mkurugenzi wako, sijui awe nani... akikuandikia barua ya uhamisho akuandikie na hundi yako ya malipo papo hapo. Bila hivyo hakuna kuhama,” alisisitiza Rais Magufuli. Alisema serikali inafanya hayo yote kwa nia njema ili watanzania wengi wapate ajira na maslahi yakipandishwe yawaguse wahusika wenyewe.
Madeni ya wafanyakazi Rais Magufuli alisema Serikaili hadi sasa imeshalipa malimbikizo ya mishahara ya kiasi cha Sh bilioni 14 na Sh bilioni 42.4 za madeni mengine. Alisema wataendelea kulipa madeni mengine kadri ya itakavyojiridhisha kuwa sio madeni hewa. Alisema kila deni wanalipima ili kujua kama ni deni halali au la. Alisema wanafanya hivyo ili kila mfanyakazi apate haki zake zote.
Hawezi kusahau alikotoka Katika hotuba yake, Rais aliwahakikishia wafanyakazi wa umma wao kama viongozi hawawezi kusahau walikotoka kwa maana nao walikuwa watumishi. “Labda wenzangu watasahau, nimezaliwa kijijini najua mateso wanayopata watumishi wa serikali, najua mnavyojitolea, wauguzi wanajitoa mhanga kuokoa maisha ya wagonjwa na wakati mwingine wagonjwa wanakutukana.
Walimu mnafanya kazi kubwa ya kuelimisha vijana wetu na baadhi ya vijana hao wana viburi hawawaheshimu ila mnajenga.... nawahakikishia Serikali yangu iko pamoja na nyinyi na wala haidharau maombi ya maslahi yenu,” alisema Rais Magufuli. Awasifu viongozi Tucta Rais Magufuli pia alitumia hotuba hiyo kuwasifu viongozi wa sasa wa TUCTA kuwa wako pale kwa ajili ya kutatua matatizo ya wafanyakazi na sio kupambana na Serikali. Alisema viongozi wenye kutaka kushindana na serikali kamwe hawezi kufanikiwa.
Aliwahoji walimu kwamba walikuwa wanakatwa asilimia mbili ya mshahara yao lakini hawafahamu ilifanya nini. “Walimu mkoa hapa mlikuwa mnakatwa asilimia 2 ya mishahara yenu iko wapi, mara nasikia imetumika kuanzishia benki, yaani kuna mambo ya ovyo ovyo tu. Kwa nini hamjamuuliza aliyekuwa anawakata kuwa kazipeleka wapi hizo fedha zenu,” alieleza.
Alisema ila viongozi wa sasa hivi wapo kwa ajili ya kujenga maana hawataki mgogoro na serikali. “Labda na wao watabadilika huko mbele, lakini tukienda hivi tutafika salama.” Aliwasifu pia Tucta kwa kukataa kuwatetea wafanyakazi wazembe, wabadhirifu, wenye majungu na wasiotaka kufuata sheria za kazi. Aliwasihi wafanyakazi kulinda amani na kupambana na dawa za kulevya.

Share :

Facebook Twitter Google+
0 Komentar untuk "RAISI MAGUFULI:WALIOGHUSHI UMRI WAJIANDAE"

Back To Top