Jana Jumanne Aprili 11, 2017 Mwenyekiti
wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Bahame Tom
Nyanduga ametoa tamko lililoambatishwa kwa vyombo vya habari kuhusiana
na matukio ya watu kutekwa na kupotea.
Soma hapa tamko hilo la Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Bahame Tom Nyanduga :
Katika siku za karibuni kumekuwepo na
taarifa katika vyombo vya habari, ikiwemo mitandao ya kijamii, kuhusu
matukio ya kupotea au kutekwa kwa wananchi katika mazingira yenye
utatanishi, suala ambalo limeibua mijadala katika jamii.
Siku ya Jumatano tarehe 5 Aprili, 2017 msanii wa muziki wa kizazi kipya, Bw. Ibrahim Mussa a.k.a
Roma Mkatoliki na wenzake watatu walitekwa wakati wakiwa katika studio
za Tongwe Records, eneo la Masaki jijini Dar es Salaam, baada ya
kuvamiwa na kundi la watu wasiojulikana. Tarehe 10 Aprili 2017 Bw.
Ibrahim Mussa alieleza mbele ya vyombo vya habari jinsi walivyotekwa na
kuteswa.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora inalaani vitendo hivyo, kwani vinaashiria kuwepo kwa makundi
yanayoendesha matendo ya utekaji watu kinyume cha sheria.
Matukio ya hivi karibuni ya kuvamia
kampuni za tasnia ya habari na mawasiliano au kuwateka watu, yanaashiria
kutoweka kwa uvumilivu wa uwepo wa maoni tofauti katika jamii kuhusu
mambo mbalimbali.
Kuna matukio yaliyowahi kutokea huko
nyuma, kwa mfano, mwandishi wa habari wa Mwananchi Communication Ltd.
(MCL) na Deutsche Welle (DW), Bi. Salma Saidi, tarehe 19, Machi 2016,
alitekwa na watu wasiojulikana Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu
Julius Nyerere, akitokea Zanzibar, na inasemekana aliteswa na kuachiwa
baada ya siku kadhaa.
Pia kumekuwepo taarifa za kutekwa Mkuu
wa Idara ya Utafiti na Sera wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) na Msaidizi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Bernard Focus
Saanane a.k.a Ben Saanane, aliyetoweka nyumbani kwake eneo la Tabata jijini Dar es Salaam Novemba 18, 2016 na mpaka sasa hajulikani alipo.
Wakati Bi. Salma Saidi na Bw. Ibrahim
Mussa na wenzake watatu walionekana baada ya muda mfupi, Bw. Ben Saanane
bado hajulikani alipo, yapata miezi mitano sasa.
Uchambuzi wa Tume unaonyesha kuwa
waliotekwa wamefanyiwa hivyo kutokana na tasnia yao, au kutumia haki yao
ya msingi ya uhuru wa maoni na kujieleza, haki ambazo zimeainishwa na
kulindwa katika Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(1977), Ibara ya 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na
Kisiasa (1966), na Ibara ya 9 ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu
na Watu (1986).
Tanzania ni nchi ambayo imeridhia na
kuafiki mikataba hiyo, na matamko mbalimbali ya kimataifa yanayosisitiza
haki hizo. Haki ya kujieleza inaweza kuhojiwa iwapo tu itatumika
kinyume na hadhi ya mtu mwingine, au maslahi ya taifa, kiusalama,
kiafya au kimaudhui, na itahojiwa kwa taratibu za kisheria
zinazokubalika katika jamii inayoheshimu demokrasia, kwa kuzingatia
Katiba ya nchi na mikataba ya Kimataifa.
Tume inapenda kusisitiza kwamba katika
nchi yenye demokrasia, serikali ina wajibu na jukumu la kuzilinda haki
hizi, na pia kuwalinda wananchi dhidi ya matendo yanayodhalilisha utu
wao, utesaji, na matendo yote yanayowanyima uhuru na haki zao za msingi,
ikiwemo haki ya maoni na uhuru wa kujieleza.
Kujirudia kwa matukio ya kutekwa watu
bila ya serikali kuwakamata wale wanaotekeleza matendo hayo, na
kuwapeleka katika vyombo vya sheria, ni jambo la kushangaza, na la aibu
kwa taifa.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora inasikitishwa kuwepo kwa vitendo hivyo katika nchi yetu ambayo
imejengeka katika misingi ya haki na demokrasia. Tume inapenda kutoa
tahadhari kwamba vitendo kama hivyo na uwepo wa makundi ya kihalifu
yanayotekeleza utekaji, utesaji,na mauaji ya watu, yaani (forced
disapperance, torture, extra judicial and summary executions) hutokea
katika nchi ambazo zinaashiria kuvunjika kwa utawala wa sheria. Vitendo
hivi havitakiwi kuvumiliwa kabisa, na Tume haipendi kuamini kwamba nchi
yetu inaelekea huko.
AHSANTE KUENDELEA KUSOMA HABARI KATIKA BLOG YETU
ILI KUPATA HABARI KWA WEPESI ZAIDI LIKE PAGE YETU YA kiraminews
IPO UPANDE WA CHINI NA UPANDE WA JUU WA KUSHOTO WA BLOG HII AU
0 Komentar untuk "TUME YA HAKI ZA BINADAMU YATOA TAMKO KUFUATIA MATAUKIO YA UTEKAJI WA WATU YANAENDELEA INCHINI "