Haya ndio alioyaongea leo bungeni soma zaidi
Tangu
mwezi Novemba mwaka 2015 nchi yetu ilipata Serikali mpya iliyoanza kazi
kwa kasi kubwa haswa katika maeneo ya kupambana na rushwa, ufisadi na
kuongeza mapato ya Serikali. Wananchi walikuwa na matumaini makubwa sana
kutokana na mwanzo huu, na hata ufanisi katika utendaji wa kazi
Serikalini ulianza kuboreka.
Bahati
mbaya, leo tunapokutana kujadili utendaji wa Serikali wa mwaka uliopita
na kupanga Bajeti ya mwaka unaofuata wa fedha matumaini hayapo tena,
kuna hali kubwa ya kukata tamaa miongoni mwa wananchi.
Maeneo
mengi ya nchi kuna uhaba mkubwa wa chakula na badala ya Serikali na
hasa Rais kuwa matumaini Kwa wananchi akiwa Comforter In Chief, kumekuwa
na maneno makali ya kuwakatisha tamaa wananchi. Bei za vyakula nchini
zimepanda mno kiasi cha wananchi kushindwa kumudu chakula ili waweze
kufanya kazi na kukuza Uchumi.
Taarifa
za Serikali kupitia ripoti za Benki Kuu zilizopo kwenye tovuti yake juu
ya hali ya Uchumi ya nchi yetu (Quartely Economic Review na Monthly
Economic Review) kwa mwezi wa Disemba 2016 zinaonesha kuwa kuna mfumuko
mkubwa mno wa bei za Vyakula, hasa Chakula Kikuu kwa Watanzania -
Mahindi, ambapo bei ya chakula hicho kikuu nchini imepanda kwa zaidi ya
30% na kupandisha mno gharama za maisha za wananchi wote nchi nzima.
Leo
bei ya kilo moja ya mahindi nchini iko sawa au ni zaidi ya bei ya kilo
moja ya mchele kwenye miji mbalimbali nchini, sukari bei juu, mafuta ya
kula bei juu nk. Kwa wakazi wa mjini hata bei ya gesi kwaajili ya
kupikia majumbani imepanda, wananchi wamerudia matumizi ya mkaa,
tujiandae na uharibifu wa misitu nchini.
Jana
Ofisi ya takwimu ya Taifa imetoa Taarifa ya kuonyesha kuwa Mfumuko wa
Bei umepanda kwa kasi na sasa umefika asilimia 6.4 Kwa mwaka unaoishia
Machi, 2017. Ibara ya 20 ya Hotuba ya Waziri Mkuu iliyosomwa bungeni
inaonyesha mfumuko wa bei wa asilimia 5.2 kwani wametumia takwimu za
mwezi Desemba, 2016.
Ukuaji
wa sekta binafsi umedorora na kushuhudia biashara maelfu kwa maelfu
zikifungwa na kusababisha ajira nyingi kupotea na ajira chache
kutengenezwa. Katka Ibara ya 26 ya Hotuba ya Waziri Mkuu inaonekana kuwa
ajira 418,000 zilizalishwa mwaka 2016/17. Lakini Waziri Mkuu
hakulieleza Taifa kuwa Hivi sasa Watanzania 1.6m wanaingia kwenye soko
la Ajira kila mwaka. Pia Waziri Mkuu hakueleza Taifa ni ajira ngapi
zimepotea Kwa viwanda kufungwa au kupunguza uzalishaji na biashara
kufungwa. Manispaa ya Ilala peke yake imefunga biashara 2900 na hivyo
kupoteza chanzo cha mapato ya Manispaa. Lakini hata mikopo ya Kibenki
kwa sekta binafsi imepungua mno, ikiwa ni kiashiria cha mdororo wa sekta
binafsi.
Matamko
ya viongozi wakuu wa Serikali kuhusu mwelekeo wa Uchumi yanatuma ujumbe
hasi kuhusu uwekezaji wa mitaji nchini, na hivi sasa kila mwekezaji
kwenye macho ya Serikali anaonekana mpiga dili. Juhudi zote za
kuhamasisha uwekaji wa mitaji nchini zilizofanywa tangu Serikali ya
awamu ya tatu, zimefutwa katika mwaka Mmoja tu wa Serikali ya awamu ya
tano. Hali ni ya kusikitisha sana.
Tatizo
jengine kubwa ni suala la ajira, ukiondoa ajira zilizopotea kwa mdororo
wa sekta binafsi, lakini pia hakuna ajira mpya serikalini tangu awamu
ya tano iingie madarakani. Vijana mbalimbali waliomaliza masomo yao ya
Ualimu, Utabibu, Maafisa Kilimo, Mifugo na Uvivu bado wako mtaani bila
ajira kwa mwaka sasa. Hata walioajiriwa mwanzoni ajira zilisitishwa kwa
kisingizio cha uhakiki wa watumishi wa Umma.
Yote
hayo yana athari kwenye uchumi wa nchi, yamepunguza kipato cha
wananchi, yamechangia ugumu wa maisha. Yamefuta matumaini waliyokuwa
nayo watanzania na yamewakatisha tamaa. Bunge letu lina wajibu wa
kuhakikisha Serikali inarelebisha hayo.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge - Kigoma Mjini (ACT Wazalendo)
Bungeni Dodoma
April 11, 2017
0 Komentar untuk "ZITTO KABWE:TANZANIA HALI YA UCHUMI IMEKUA MBAYA SANA NA ATHARI ZAKE NI UKOSEFU WA AJIRA NA UGUMU WA MAISHA "