Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amezungumzia sakata
la makontena ya mchanga unaodaiwa kuwa na madini uliozuiwa katika
Bandari ya Dar es Salaam, akisema madini mengine yaliyomo humo siyo mali
ya Tanzania.
Lissu amesema kwa maoni yake Serikali haipaswi kuzuia madini hayo
kusafirishwa kwenda nje kwa kuwa ni kukiuka mikataba na sheria ya
madini.
“Hili halizungumzwi kabisa na liko katika mikataba. Madini mengine si
yetu kwa sababu haihesabiwi katika asilimia mia ya dhahabu,” amesema
mwanasheria huyo wa kujitegemea alipotembelea ofisi za Mwananchi.
Mbunge huyo amesema kwamba, kwa hoja za kodi Taifa halina chake katika
suala la madini, isipokuwa ni asilimia nne ya pato inayolipwa na
mwekezaji kama mrahaba kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 1998.
Lissu ameongeza kuwa sheria hiyo inampa mamlaka mwekezaji kuwa, iwapo
anapatiwa leseni ya uchimbaji kile anachopata ardhini kinakuwa ni mali
yake.
“Haki yetu ni asilimia nne tu ya mirabaha. Kwa kifupi, kwenye madini tumewapa (wawekezaji) madini bure, tena kisheria,” amesema.
Mwanasiasa huyo amesema anashangaa kuona mchanga unazuiwa bandarini
wakati Rais John Magufuli alikuwa katika Baraza la Mawaziri wakati
Sheria ya Madini ya mwaka 1998 na 2010 zikipitishwa.
0 Komentar untuk " TUNDU LISU- MADINI MENGINE SI MALI YA TANZANIA KISHERIA "